
Kaunti ya Nakuru Yakuza Sanaa, kama Kitega Uchumi Miongoni mwa Vijana
Imeandikwa na James M Alumera na Nyasimi Dawson
Afisa Mkuu wa vijana ,michezo na talanta kaunti ya Nakuru Alex Maina, amewapa changamoto wasanii, akiwataka kutumia fursa zilizopo, ili waweze kufaidi na kuendeleza usanii wao.
Akizungumza wakati wa kikao na wasanii katika ukumbi wa sanaa wa Nakuru maarufu kama Nakuru players theatre , amehimiza usimamizi wa kituo hicho cha sanaa, kufanya makubaliano kati yake na serikali ya kaunti ya Nakuru kwa lengo la kupiga jeki sanaa na ubunifu katika eneo hilo, kitaifa na hata kimataifa.
Mkurugenzi wa sanaa katika kituo hicho Barbushe Maina amesisitiza haja ya kukuza vipaji vya wasanii wa sasa, na kwa wanaochipuka.
Licha ya changamoto za usafiri na garama ya malipo mengine kituoni humo, wasanii hao wanasema imekuwa vigumu kwao kusafiri hasaa wanapohitajika kwenda kuigiza na kutoa mafunzo katika sehemu zingine.
Kadhalika Maina anasema japo kumekuwa na matumizi ya sana ya lugha ya kiingereza kwa wasanii wanapoigiza , amewahimiza kukumbatia matumizi ya lugha ya Kiswahili kama kiungo muhimu cha kupitisha na kufanikisha jumbe mbalimbali kama vile za uongozi na utawala bora, maadili ya kijamii, nidhamu, na usalama, kwa jamii kwa ujumla.
Mkuu wa mauzo wa kituo hicho, Simon Thuo , anasema kwa sasa jukwaa lao la mitandaoni halijaimarishwa inavyostahili.
Thuo anasema jukwa hilo likiboreshwa zaidi litawavutia wengi na wataweza kujua na kujitokeza kutoka sehemu tofauti za nchi na kuja kutazama baadhi ya michezo ya kuigiza katika kituo hicho.
Fursa hiyo ikitoa nafasi ya kujipatia kipato, kitakachowafaidi wasanii hao na kwa maendeleo ya kituo hicho, kwa hali na mali.
Ni matamshi yanayojiri, kituo hicho kikijiandaa kwa onyesho la mchezo wa kuigiza, ‘Natala’, mnamo tarehe 15 mwezi Aprili.mwaka huu.
Siku hiyo ikiambatana na siku ya Sanaa duniani, wanamwomba Gavana Susan Kihika kuhudhuria na kujionea mchezo huo.